Sunday, August 28, 2016

MBUNGE WA JIMBO LA ILEMELA AFANYA ZIARA NA KUTEKELEZA SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI































MBUNGE WA JIMBO LA ILEMELA AFANYA ZIARA NA KUTEKELEZA SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline S.L Mabula akiambata na viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa wilaya ya Ilemela na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Amefanya  ziara katika maeneo mbalimbali ikiwa ni juhudi za utekelezaji wa Ilani na kutatua changamoto mbalimbali katika kuwaletea wananchi wa wilaya hiyo maendeleo.
Mbunge huyo alianza ziara yake kwa kutembelea soko la Kirumba ambapo alikagua na kuzungumza na wafanyabiashara wa eneo hilo waliokumbwa na mkasa wa kuharibiwa mali zao walizokuwa wanauza sokoni hapo na mgambo wa Halmashauri huku akilaani kitendo hicho na kuitaka Halmashauri kuwapa kifuta jasho wananchi hao kufuatia kujitokeza kwa uharibifu huo.
Aidha ameitaka Halmashauri kuyapitia upya masoko yake na kuboresha mazingira yake kabla ya zoezi la kuwahamisha wafanyabiashara hao.
Wakati huo huo Mbunge huyo alipata wasaa wa kuitembelea shule ya sekondari ya Wavulana Bwiru nakugawa madawati elfu moja (1000) kila dawati likiwa na thamani ya laki moja ikiwa ni jitihada za ofisi yake katika kuunga mkono sera ya serikali ya awamu ya tano ya upatikanaji wa elimu bure na kuwasaidia wanafunzi kuweza kupata elimu bora ili kujiletea maendeleo na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Aidha Mbunge huyo pia amepokea msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo mabati mia saba na nne (704) na simenti mifuko mia tatu (300) kutoka kwa shirika la Nyumba la Taifa ( NHC ) ikiwa ni jitihada za shirika hilo katika kuunga mkono agizo la Mhe Rais Magufuli na Mbunge wa Jimbo hilo katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kupata elimu bora.
Pamoja na kushukuru  Mbunge huyo ameitaka NHC kuwa wadau endelevu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya watu wote huku akiwaasa madiwani wa Jimbo hilo kuanza harakati za kuchochea  utengenezaji wa madarasa kwa kuwa mwarobaini wa pahala pa kuweka madawati umeshapatikana.
Nae meneja  wa shirika hilo mkoa wa Mwanza  amesema kuwa hakuna taifa lolote duniani lililoendelea kwa watu wake kukosa elimu hivyo kuyataka mashirika na taasisi nyengine kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo.
Hata hivyo kampuni ya Rangi ya Coral Paint nayo imetoa msaada wa ndoo za rangi zenye zaidi ya thamani ya shilingi milioni moja, laki tatu na elfu nane katika kuunga mkono jitihada za mbunge huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Ilemela alieambatana na mbunge huyo amempongeza kwa jitihada zake za kuwatumikia wananchi wa wilaya hiyo huku akiahidi kumpa ushirikiano katika kuwaletea wananchi maendeleo na kusema kuwa ''.. Sitamvumilia mtendaji yeyote au mkuu yeyote wa idara atakaekwamisha shughuli za maendeleo na naagiza kuanzia leo watendahi wote ambao hawatasimamia vizuri shughuli za maendeleo zitazofanyika kwenye kata zao na ukatokea ubadhirifu basi mimi ntaanza na hao kwanza huku tukiwatafuta wahusika wengine..'' akisisitiza.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kuona hao ni sehemu ya shughuli za kimaendeleo na kuwataka  waunge mkono jitihada za serikali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Ilemela Ndugu John Wanga amempongeza mbunge huyo kwa jitihada zake tangu changamoto ya madawati mpaka sasa kwenye hatua za uanzaji wa utengenezaji wa majengo ya madarasa ili kuwawezesha watoto kupata elimu bora  na kuahidi kusimamia vizuri mali zote na michango ya shughuli za maendeleo.
''ILEMELA NI YETU TUSHIRIKIANE KUIJENGA''
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge.
Jimbo LA ilemela-Mwanza.

0 comments:

Post a Comment