Thursday, August 18, 2016

MGOGORO WA ARDHI KIRUMBA WATATULIWA












Hatimae serikali imetegua kitendawili kuhusu hatma ya wananchi wa mitaa ya Kabuhoro, Songambele na Kigoto kata ya Kirumba wilaya ya Ilemela kwa kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na jeshi la polisi kwa kubatilisha agizo la jeshi hilo lililowataka wananchi wa mitaa hiyo kuhama eneo hilo ndani ya siku saba.

Hayo yamebainishwa leo na Ndugu James Chuwa kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo alipokuwa akitoa kauli na msimamo wa  serikali kuhusu hatma ya wananchi hao kufuatia agizo hilo la muda mfupi lililowataka wananchi hao kuhama eneo hilo ndani ya siku saba huku kukiwa hakuna njia mbadala ya kuwasaidia wananchi hao  ikiwa ni pamoja na kuwapa muda wa kutosha sanjari na kuwaonyesha eneo sahihi la kuishi.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo amesema "...  Zoezi la kuhama ndani ya siku saba  haliwezekani na halipo kwa sasa na zaidi Mhe mkuu wa wilaya ameshaitisha kikao cha dharula cha kamati ya ulinzi na usalama mapema  Agosti 22 mwaka huu kuona namna bora zaidi ya kulimaliza suala hili",  huku akiwasisitiza wananchi kulipia kodi za majengo ili waweze kujiletea maendeleo.

Wakati huo huo katibu wa mbunge kwa niaba ya mbunge wa jimbo la Ilemela   Ndugu Kheri James ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka na makusudi katika kutatua tatizo hilo huku akiiasa kuzingatia utu na ubinadam kwa wananchi hao.

Nae amesema ".. wananchi hawa ni masikini na wengi wanaoishi hapa ni wazee na wajane  kitendo cha kuwaambia wahame ndani ya siku saba ni kuwaonea bure hawatakuwa na uwezo hata mtu mmoja wa kwenda kujenga kwengine haliyakuwa wameshindwa kulipia maeneo ya biashara mjini kulikopelekea Mhe Rais kuwasamehe na kubaki kufanya biashara maeneo ya  mjini., Naiomba serikali kama iliwasamehe masikini hawa kufanya biashara zao kwa kigezo cha umasikini wao basi iwasamehe tena waweze kuishi ndani ya eneo hili.." alieleza.

Aidha mgogoro huu ulianza kwa jeshi la polisi kufika maeneo hayo na kuwataarifu kuwa eneo wanaloishi ni eneo la jeshi hilo mapema July 19 mwaka huu na baadae kubandika matangazo yanayowataka wananchi hao kuhama eneo hilo ndani ya siku saba.


Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo kwa niaba ya wananchi wote ameishukuru ofisi ya mkuu wa wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge katika kutafuta suluhu ya tatizo hilo huku akisisitiza upatikanaji wa  ufumbuzi wa haraka kuepusha vurugu na vitendo visivyo vya kibinadamu kujitokeza kupitia mgogoro huo.

NB;  Ikumbukwe kuwa maamuzi haya ni matunda ya maombi yaliyofanywa na mbunge wa jimbo Mhe Dkt. Angeline Mabula kwa mkuu wa wilaya kwa niaba ya wananchi.

"ilemela ni yetu,tushirikiane kuijenga "
  Imetolewa na Ofisi ya Mbunge.
 Jimbo LA ilemela-Mwanza.
 

0 comments:

Post a Comment