Jimbo la Ilemela limepokea msaada wa mifuko 200 ya Saruji kutoka kwa Ndugu Zuli Nanji mmiliki wa Mwanza Huduma katika kuunga mkono jitihada za Mhe Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ili kuhakikisha yanaboreshwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia
Akizungumza katika makabidhiano hayo Bwana Zuli Nanji amesema kuwa ameamua kutoa msaada huo kwa Mbunge wa Ilemela kufuatia kuguswa kwake na juhudi zinazofanywa na Mbunge huyo katika kuboresha Elimu kwa wananchi sambamba na kuwataka wafanyabiashara wengine na watu wenye uwezo kuunga mkono jitihada zote za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii zinazowakabili wananchi
'…Mifuko 200 ya Saruji naitoa kwa moyo mmoja katika kumuunga mkono Mhe Mbunge wa Ilemela kwa jitihada zake anazozifanya za kutatua matatizo ya wananchi, Ninawaomba watu wengine wenye uwezo wamuunge mkono…'
Kwa upande wake Mhe Mbunge wa Jimbo la Ilemela amemshukuru Ndugu Nanji kwa kuguswa kwake na kuamua kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazofanywa ndani ya Jimbo la Ilemela huku akiwakumbusha wananchi kuwa sehemu ya maendeleo hayo kwa kutimiza wajibu wao kama wazazi katika kufanikisha adhma ya Serikali ya Elimu bila malipo
'…Zoezi hili la uchangiaji wa Elimu ni endelevu tulianza na madawati sasa tupo kwenye vyumba vya madarasa tukishirikiana Mhe Mkuu wa Wilaya, Mstahiki Meya, Mkurugenzi, na Mbunge tunatimiza wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake lakini na wananchi wanao wajibu katika hili niwaombe mtakapofikiwa na jambo hili msituangushe…'
Mhe Mbunge pia amezitaka shule zote zilizokwisha anza kunufaika na vifaa vya ujenzi wa Madarasa, Zahanati, na Huduma nyengine za Jamii kutoka Ofisi yake kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa
Wakati huo huo Ziara za Mbunge kwa Kata za Jimbo hilo zimeendelea akiambatana na Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela, Mkuu wa Wilaya, Mstahiki Meya, Mkurugenzi na wataalamu wa Manispaa ambapo siku ya jana walifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Ibungilo na leo watakuwa Kata ya Nyasaka kusikiliza Kero za Wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa papo kwa hapo sambamba na kuhamasisha maendeleo
' Ilemela ni yetu,Tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
20.12.2016
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
20.12.2016
0 comments:
Post a Comment