Wednesday, March 8, 2017

WAWAKILISHI WA WANANCHI WATAKIWA KUYASIMAMIA MASLAHI YA WANAWAKE






Wawakilishi wa wananchi kwa ngazi mbalimbali za Uongozi wametakiwa kuyasimamia na kuyaweka mbele maslahi ya wanawake wanapokuwa katika vikao vyao vya maamuzi     

Hayo yamebainishwa leo na Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokuwa akizungumza na Wanawake wa Mkoa wa Mwanza katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za siku ya Wanawake Duniani yakiwa na Kauli Mbiu kuwa Tanzania ya Viwanda 

Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko Kiuchumi ambapo kimkoa yamefanyika Viwanja vya Furahisha wilayani Ilemela yakitanguliwa na Maandamano ya amani kutoa Viwanja vya Shule ya Sekondari Baptist

Akizungumza katika maadhimisho hayo MheshimiwaDkt Mabula amesema kuwa umefika wakati kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuweka maslahi ya Wanawake mbele na kuyasimamia ili kulikwamua na kulisaidia kundi hili kubwa linalonyanyaswa na kuonewa katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo

Aidha amewasisitiza Viongozi wanawake waliopata fursa kuwa mbele katika kuhakikisha wanasaidia wanawake wenzao na watoto ili kuzifikia ndoto zao

‘… Niwatake viongozi wenzangu mnapokaa katika vikao vya maamuzi jicho lako la kwanza litazame nini kimetengwa kwa maslahi ya wanawake wa eneo lako, Tega masikio ni kipi kipo kule na Sisi tuliopewa nafasi lazima tuoneshe kuwa tunaweza kwa kuweka wanawake wenzetu mbele …’

Aidha amewataka wanawake kuwekeza katika fursa tofauti tofauti za kiuchumi zinazojitokeza ikiwemo ununuzi wa hisa za makampuni nchini

Nae Marry Mhoha akisoma risala kwa niaba ya wengine ametaka kupewa kipaumbele kwa wanawake katika nafasi za Uongozi kuhakikisha wanayatatua matatizo yao kupitia nafasi hizo

Akihitimisha Sherehe hizo Mbunge wa Viti Maalum kupitia Mkoa Mwanza Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma amemshukuru Daktari Mabula kwa kujumuika pamoja nao na kumhakikishia kuwa wanatambua mchango wake ktk kuwatumikia wanawake na jamii kwa ujumla


Imetolewa na

Ofisi ya Mbunge 
Jimbo la Ilemela
08.03.2017

0 comments:

Post a Comment