Wednesday, April 5, 2017

KAMATI MAALUMU YA JESHI LA WANANCHI YA KUBAINI MIPAKA YAANZA KAZI





Kamati maalumu ya Jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ kutoka makao makuu ikiongozwa na mkuu wa kikosi cha Anga 601 Meja BM Msilu imeanza kazi rasmi leo ya kubaini upya mipaka ya jeshi hilo ili kumaliza sintofahamu ya kimipaka baina ya jeshi hilo na wananchi wa maeneo jirani.

Mbali na Jeshi kamati imejumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Katibu wa ofisi ya Mbunge Jimbo la Ilemela, Kaimu Katibu Tawala wa wilaya Ilemela, Afisa Ardhi Kanda ya Ziwa na Wapima Ardhi kutoka Halmashauri ya Manispaa Ilemela.

Aidha kuanza Kazi kwa kamati hii ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt Angeline Mabula aliyoitoa  mapema mwanzoni mwa mwaka huu alipokuwa akizungumza na wananchi wa maeneo yanayokabiliwa na migogoro ya mipaka na kuahidi kuyashughulikia haraka iwezekanavyo ili kutoa fursa kwa wananchi wa maeneo hayo waweze  kuendelea na shughuli za kujiletea maendeleo sanjari na kuepusha changamoto zinazoweza kuchochewa na migogoro hiyo .

Akizungumza katika zoezi hilo Afisa wa Ardhi kutoka Kanda ya Ziwa Bwana Eliah Kamihanda amesema
‘… Kazi yetu kubwa ni kubaini uhalisia wa mipaka ya Jeshi na wananchi ili baada ya Zoezi kutoa fursa ya maamuzi yenye haki na usawa kwa pande zote mbili kwa lengo kusaidia utatuzi wa migogoro ya mipaka …’ 

Nae Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Kheri James amesema kuwa  lengo la Mhe Mbunge pamoja na Uongoz wa wilaya ni kuona migogoro yote ya Ardhi ndani ya Jimbo kati ya Wananchi na Taasisi au Wananchi na Wananchi inakwisha,  

Hivyo hizi ni sehemu ya Juhudi  za Mhe Mbunge kwa kushirikiana na Mamlaka nyengne kuona migogoro hiyo inakwisha, Tunawasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa kamati inapopita katika maeneo yao sambamba na kujiepusha na manunuzi au matumizi ya ardhi bila kufuata taratibu 


Imetolewa na 
Ofisi ya Mbunge 
Jimbo la Ilemela
04. 04. 2017

0 comments:

Post a Comment